5 Apr 2016

MFAHAMU ' JUMANNE NGOMA ' ,MTANZANIA ALIYEGUNDUA MADINI YA TANZANITE NA GYPSUM.

pichani alievaa suti ni bwana jumanne ,mgunduzi wa tanzanite.


Mzee Jumanne Ngoma ndiye mvumbuzi wa madini haya, mwenye shahada ya Uvumbuzi alizotunukiwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika maandhimisho ya sherehe za Mei Mosi Mbeya mwaka 1984.

Mzee Jumanne Mhero Ngoma (Mvumbuzi) wa madini haya ya Tanzanite, alizaliwa mwaka 1939 katika kijiji cha Marwa wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.
Wazazi wake walikuwa wafugaji wa Ng’ombe na mbuzi hivyo waliishi maisha ya kuhamahama ili kupata malisho bora ya mifugo kama ilivyo hulka na tabia za wafugaji.

Wakati akiendelea na shule ya msingi,  mwaka 1952 wazazi wake walihama kutoka Hedaru na kwenda kuishi Mererani. Mzee Jumanne Mhero Ngoma, aliweza kusafiri na wazazi wake hadi Mererani, akaendelea na masomo yake katika shule iliyokuwa ikiitwa Town School iliyopo Arusha mjini, ambako ilibidi akae na mjomba yake, Ruben Mkali aliyekuwa akiishi Arusha Mjini wakati huo.

Mwaka huo 1965, alifunga ndoa na Bi Fatma Mauya, na kupata watoto nane

Mzee Jumanne Ngoma alijiunga na kozi fupi ya madini iliyokuwa ikitolewa na Wizara ya Madini wakati huo. Baada ya kumaliza kozi ya madini katika ofisi ya madini Morogoro, Juni 1, 1966 alipata leseni ya madini baada ya kuhitimu mafunzo hayo.

Siku chache baada ya kumiliki leseni ya utafiti wa madini, Mzee Jumanne Mhero Ngoma alirejea nyumbani kwake Makanya.

Alipokuwa Makanya aliamua kuanza utafiti wake kijiji chake cha Makanya. Mzee Ngoma aliaza shughuli za utafiti wa madini, ndipo akagundua Madini ya Gypsum, na kuwa mtu wa kwanza aliyegundua Gypsum maeneo ya kijiji cha Makanya, sasa hivi eneo hilo linaitwa Chang’onko

Hivyo alipopata elimu hiyo ya madini aliamua kwenda Meralani, katika eneo la Lalouo kijiji cha Naisunyai kufanya utafiti wa yale mawe aliyoyaona wakati anachunga mifugo ya baba yake. Mwaka 1967 Januari, aliamua kuyapeleka mawe yale katika ofisi ya madini Moshi kwa uchunguzi. Alishauriwa na afisa wa madini kipindi hicho Bwana Bills, ofisi ya madini Moshi ikayapeleka kwenye maabara ya taifa Dodoma kwa uchunguzi zaidi.

Mnamo tarehe 23 Septemba 1967 maabara ya Dodoma ilithibitisha kuwa ni madini ya Zoisite ambayo kwa wakati huo hayakuwa na soko, lakini wakashauri huenda yakawa na soko siku zijazo.

Mnamo Mwaka 1984, Serikali ya Jamhuri ya muungano ilipotambua rasmi Mvumbuzi ya madini hayo na kuyapa jina la “TANZANITE” jina lililotokana na jina la nchi, yaani Tanzania na Zoisite na likapatikana jna hilo. Hapo alimtunukia cheti cha uvumbuzi katika sherehe ya siku ya wafanyakazi zilizofanyika mkoani Mbeya.

Kutokana na historia fupi hii ya uvumbuzi wa madini haya,   tayari kuna asasi ya  kuenzi jitihada za mvumbuzi huyu wa madini pekee yanayopatikana Tanzania pekee.

Asasi hii mpya ya kiraia itakua inajulikana kwa jina la TANZANITE FOUNDER FOUNDATION, kwa kifupi “TAFFO”, ambayo yeye (mvumbuzi) ni mmoja wa waanzilishi wake.

TAFFO ni asasi isiyo ya kiserikali itakayojishughulisha na wachimbaji wadogo wadogo wa madini vijana, wanaofanya shughuli za madini yote yanayopatikana ndani ya nchi yetu ya Tanzania yakiwemo TANZANITE.


Malengo makubwa ya asasi hii ni:

1. Kuwawezesha vijana kupata utaalam (elimu) katika sekta ya madini.

2.Kuwawezesha kupata nyenzo za uchimbaji madini kutoka vyanzo mbali mbali ikiwemo Serikali, mashirika ya ndani na nje ya nchi, Asasi, mabenki na Mtu mmoja mmoja atakayeguswa na huduma za asasi hii.

3.Kuenzi na Kuhifadhi historia ya uvumbuzi wa madini ya TANZANITE kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.


Taasis hiyo imeshukuru serikali kupitia wizara ya Nishati na Madini na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kwa kuwawezesha kapata usajili wa asasi hii.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni