3 Apr 2016

HUU NDIO MCHANGA UNAOTEMBEA KWA KUHAMA HAMA NDANI YA HIFADHI YA NGORONGORO.







“Mchanga huu unaaminika kuwa ni matokeo ya mlipuko wa volcano kwenye mlima wa Oldonyo Lengai uliorushwa maeneo karibu na mlima uliokuwa kwenye eneo la Kreta ya Ngorongoro karibia miaka 3,000 iliyopita  lakini baadaye mlima huo ulizama na kutengeneza mbonde la Ngorngoro maarufu kama Kreta tunalolishuhudia hivi sasa,” anasema Melita amabe ni Afisa wa hifadhi hii ya Ngorongoro.







Afisa Uhifadhi huyo aliwaambia wandishi wa habari waliotembelea eneo hilo katika moja ya ziara zinazoandaliwa na kuratibiwa na NCAA kwa lengo la kuwapa upeo mkubwa wa kuelewa vivutio vinavyopatikana ndani ya hifadhi hiyo kuwa inaaminika mchanga huo wenye nguvu za uvutano ulianza safari yake katika muda usiojulikana kutokana na kutokuwepo takwimu sahihi za safari hiyo kwa miaka ya nyuma .







Ziara ya mchanga huo kwa mujibu wa Melita ulianza kupimwa rasmi mwaka 1969 ambapo vipimo vinaonyesha hutembea kwa wastani wa kiliomita 0.19.







Mchanga huo hutembelea kwa kusukumwa na upepo huku ukiwa umejikusanya pamoja bila kuacha mabaki nyuma kiasi kwamba mtu mgeni hawezi kujua ulipokuwa kipindi kilichopita hadi aelezwe na wenyeji.







Kwa sasa muonekano wa mchangao huo ni kama vile umetengeneza umbo la mlima wenye urefu wa mita 10 kwenda juu na upana wa mita 100 sawa na uwanja wa mpira wa miguu.







Maajabu mengine ya mchanga huo ni mabadiliko yanayotokea kipindi cha kiangazi na masika ambapo urefu wake hubadilika hadi kufkia mita 17 wakati upana huwa mita 45.
 



“Kati ya miaka ya 1970 na 1980 mchanga huu ukiwa katika umbo la mlima ulikuwa ukielekea upande ilipo hifadhi ya Serengeti na pale kuna mto unaopitisa maji hivyo mwaka 1991 mchanga huo ulipokuwa ukiukaribia mto huo tulianza kuumiza vichwa tukihofia kuwa utazama mtoni na hivyo kuwa mwisho wake,” anasema Melita







Anase,a hofu hiyo iliyeyuka mwaka 2000 kipindi cha mvua za El Nino ambapo ghafla mchanga huo ulibadili uelekeo kwa kuacha kwenda hifadhi ya Serengeti na badala yake kuchukua mkondo unaoelekea eneo la Enduleni.







Kwa mujibu wa vipimo vya kitaalamu, inaaminika hivi sasa mchanga huo unaelekea kwenye milima ya Ngorongoro upande wa mkoa wa Shinyanga ambapo ni eneo salama.







Hata hivyo kwa mujibu wa Melita, hivi sasa mchanga huo umegawanyika katika makundi mawili tofauti, moja ambalo ndilo kundi kunwa unaelekea milima ya Ngorongoro wakati ule mdogo bado unachukua mkondo unaoaminika kuelekea hifadhi ya Serengeti.







Maajabu mengine yanayoambata na mchanga huo ni kitendo cha mimea yote iliyo katika mkondo unakoelekea kukauka kabla hazijafikiwa lakini mara baada ya mchanga kupita eneo hilo hupata rutuba inayostawisha mimea mipya na hivyo kurejesha uoto wa asili ndani ya Kreta.







Melita anasema kuwa hakuna utafiti uliofanyika mpaka sasa kubaini sababu ya maeneo yaliyopita mchanga huo kukauka huku maeneo hayo yakionekana kuwa na rutuba baada ya kipindi kirefu kupita na majani kuanza kuchipua upya .







Kutokana na maajabu ya mchanga huo, nadhani kuna haja ya mamlaka husika kubadili namna na mfumo wa kuutangaza kutokana na kutofahamika sana miongoni mwa wageni wanaotembelea hifadhi ya Ngorongoro nikiwemo mimi mwenyewe ambaye awali sikuvutiwa sana kwenda kuutembelea hadi nilipofika na kujikuta nikiushangaa mlima mzuri uliotengenezwa kwa mchanga mweusi kabla kujulishwa kwa huo ndio mchanga wenyewe unaotembea.







Mvuto unaopatikana kwa yeyote anayefika eneo hilo ndilo lilinifanya kuwa mtu wa kwanza kukimbilia kuushika mikononi mchnaga huo lakini nikakumbana na maajabu mengine kwani ukiushikilia kwa muda mikononi mchnagao huo huishia na utajikuta huna kitu mkononi.







Mlima huo unaotengenezwa na mchanga laini hunavutia kila unapopiga hatua kuukwea kwani huacha alama za hatua unazopiga lakini ukibahatika sehemu ya mchanga kuingia ndani ya viatu vyako utajikuta ukikumbana na maajabu mengine kwani michanga hiyo hutoka yenyewe huku miguu yako ikibaki safi kana kwamba umejipangusa na kitambaa.







Nadhani muda sasa umefika kwa maelezo ya eneo hilo lenye upepo mkali lakini usiochukiza kutokana na mvuto wa mandhari yake ubadilishwe na kuitwa mlima unaotembea badala mchanga unaotembelea.







Jina hili siyo tu kwamba utaelezea uhalisia wa jambo lenyewe kutokana na mchanga huo kutengeneza kijimlima lakini pia utavutia watu kutoka ndani na nje ya nchi kwenda kuutembelea mlima unaotembe.







Pamoja na maajabu hayo ya kisayansi, lakini kuna sayansi nyingine ya kijadi kwa watu wa jamii ya wafugaji wa Kimaasai ambao wanaamini mchnaga/mlima huo una nguvu ya uponyaji na utatuzi wa matatizo mbalimbali ikwemo upatikanaji wa mimba kwa wanawake wenye tatizo ka kutopata watoto.







“Wamaasai wanaamini eneo ulipo mchanga huo ni patakatifu hivyo huenda hapo na maziwa na kufanya tambiko yao ya kijadi na wana fanikiwa kwenye yale wanayoyaomba kutokana na imani zao,” anasema Melita







Kwa mujibu wa Meneja Uhusiano wa NCAA, Adam  Akyoo, watu wengi hasa watalii wamekuwa na shauku ya kujua nini mwisho wa safari ya mchanga huo mwepesi wenye rangi nyeusi ambao hata ukiushika mkononi hutoweka na kurejea ulipoutoa baada ya muda mfupi.







Akyoo aliyekuwa ameongozana na waandishi waliotembelea hifadhi hiyo alikiri hoja kuwa mchanga huo haujatangwa vya kutosha kwa sababu siku za nyuma milima ulipo mchanga unaotembea ulikuwa kwenye maeneo ya mambo ya kale na hivyo NCAA hawakuwa na mamlaka ya kuutangaza hadi pale ulipoingia kwenye eneo la Mamlaka ndipo walipoanza kuutangaza kote duniani na watu kuanza kumiminika kuja kuutembelea.







Meneja Uhusiano huyo anabainisha kuwa NCAA wanatarajia wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi watamiminika kutembelea mchanga huo kutokana na muitiko unaoapatikana kila wanapoelezwa maajabu hayo. Nadhani huu ni muda sasa kwa watanzania wengi kutembelea Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kushuhudia maajabu haya badala ya kubaki wasikilizaji na kuacha wageni wakifaidi urithi huu tuliojaliwa na Mwenyezi Mungu.
Watalii wakiwa juu ya mchanga huo

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni