3 Jun 2016

KIFAHAMU KWA KINA KIMONDO KILICHODONDOKA TANZANIA,MKOANI MBEYA WILAYANI MBOZI.

TANGU zamani, jamii nyingi duniani zimekuwa zikivichukulia vimondo kama vitu vitakatifu, jamii hizo ni pamoja na Wanyiha wa Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya. Katika jamii zingine duniani imani hizo zimepewa taswira chanya wakati hapa nchini zinapewa taswira hasi.
Wanyiha waliamini katika utakaso kupitia kimondo hicho, imani ikajengeka ya kuosha nyota, lakini baadhi ya watu wakaihusisha zaidi na ushirikina au kuielezea kuwa ni imani potofu, lakini kwa wenyeji wanaamini chuma hicho ni Baraka kutoka kwa Mungu, kama zilivyo jamii zingine duniani.
Vyanzo mbali mbali vya taarifa za kimondo hicho zinabainisha kwamba, tangu kugunduliwa kwake, maelfu ya miaka iliyopita, wenyeji, ambao ni jamii ya kabila la Wanyiha, waliamini kuwa chuma hicho ilikuwa ni zawadi toka kwa Mungu, kwamba hiyo ilikuwa ni Baraka kwao, walizopewa na Mwenyezi Mungu.
Mtazamo huo wa wenyeji, unathibitisha jambo moja la msingi, kwamba imani yao kuhusu kimondo hicho inahusiana na Uungu na sio ushirikina au imani potofu kama inavyoenezwa na baadhi ya watu.
Kuosha nyota na utalii
Mtaalamu wa masuala ya utalii, Fanuel Sabini anaiangalia imani hiyo kwa mtazamo chanya, ambapo anasema ikitumika (imani) vizuri, itachangia kwa kiwango kikubwa kuvutia watalii wengi zaidi badala ya kuiangalia katika mtazamo hasi, kama vile kuijumuisha katika kundi la imani potofu.
“Nchi nyingi zimetumia imani hizo kuvutia watalii, mfano kuna nchi watu hutembelea kwenda kunawa maji tu, ni ya kawaida sana lakini watalii wanamiminika kwa ajili hiyo tu,” anasema Sabini, kisha anahoji,
“Kitendo hicho cha kunawa maji kina tofauti gani na kuosha nyota kwa kunawa maji yaliyowekwa kwenye kimondo cha Mbozi!”
Wadau wa masuala ya utalii wanaitazama imani hiyo ya wenyeji kuhusu kuosha nyota kwa mapana zaidi, kwamba ikitumika pamoja na utoaji elimu ya unajimu itakifanya kimondo hicho kuwa chanzo muhimu cha mapato yatayotokana na watalii wa nje na ndani.
Sabini anaielezea hatua ya kwanza na ya haraka inayotakiwa kufanyika kuwa ni kuanzishwa kwa makumbusho na kituo cha utafiti kuhusu masuala ya unajimu (astronomy), na wakati huo huo kuitangaza imani ya kuosha nyota, na kwa kufanya hivyo, eneo hilo litakuwa kitivo muhimu cha elimu ya vimondo na unajimu barani Afrika.
Vimondo na imani za dini kubwa
Imani zenye kuhusisha vimondo na nguvu za Kimungu haipo kwa jamii hiyo ya kabila la Wanyiha pekee, bali zipo katika jamii za mataifa mbali mbali duniani, ambako vilianguka. Nyingi ya imani za kidini za jamii hizo zinaelezwa kujengwa kwenye matukio ya kuanguka kwa vimondo.
Historia ya vimondo, kama inavyochambuliwa kwenye mtandao wa http://www.meteorite.fr/en/basics/history.htm(link is external) inabainisha pia jinsi vitu hivyo toka angani pamoja na matukio yanayoambatana navyo, vinavyobeba imani ya dini nyingine kubwa duniani.
Inabainishwa na watalaamu wa masuala ya vimondo kwamba kutokana na imani walizonazo jamii mbali mbali kuhusu vimondo hivyo, wamevihifadhi na imani zao kupewa mtazamo chanya, jambo ambalo limezisaidia jamii hizo kuingiza mapato makubwa kupitia utalii.
Imani hizo zimekuwepo tangu zama za kale, ambapo vimondo viliaminika kuwa vitu vitakatifu na jamii mbali mbali za wakati huo duniani.
Mazingira ya kuanguka kwake hapa duniani, ambapo huambatana na mwanga mkali, sauti, kama vile nyota idondokayo, vumbi na kishindo, ni matukio yenye kusababisha hofu kwa wale walioshuhudia, wakiamini kusababishwa na nguvu iliyo juu ya uwezo wa mwanadamu.
Vitu hivyo au hayo mawe, vilihifadhiwa na jamii vilipodondokea, kama vitu vitakatifu, na wenyeji wakayafanya maeneo hayo kuwa matakatifu, wakaabudu na kuyatumia katika shughuli zao mbali mbali za imani zao.
Tafiti mbali mbali zilizofanywa, zinathibitisha imani hizo kuwepo kwa karne kadhaa, ni tangu zama za kale. Ni imani zinazojengwa kutokana na mazingira ya uangukaji wa vimondo hivyo, ambapo huambatana na mwanga mkali na kishindo.
Lilikuwa tukio lenye maajabu kwa mwanadamu wa zama za kale, na hata leo hii, kwa mwanadamu wa kawaida yatakuwa maajabu toka kwa Mungu. Hata hivyo, kwa wanasayansi, wao wanatoa maelezo tofauti yenye majibu ya kitafiti zaidi.
Miongoni mwa simulizi za kiimani inayotumiwa na wanasayansi, ni ile inayomhusu Mtume Paul, https://www.newscientist.com/.../mg22630183-700-falling-(link is external), ambapo inaelezwa kwamba takribani miaka 2000 iliyopita alikutana na tukio lililobadili kabisa mwelekeo wa maisha yake ya kiimani, na inaaminika kuwa ni tukio lililobadili pia hata maisha ya kiimani ya wanadamu wa leo.
Uchambuzi wa tukio hilo unaegemea zaidi katika maandiko yaliyomo kwenye kitabu cha Matendo ya Mitume, Mlango wa tisa, ambapo inaelezwa kuwa mtu aliyefahamika kwa jina la Saul wakati huo, akiwa njiani kuelekea Damascus, nchini Syria aliona mwanga mkali angani, akapofuka macho na kusikia sauti ya Yesu. Baada ya tukio hilo alibadili jina, akaitwa Paul, na akajiunga na Ukristo.
Hatua hiyo ya Mtume Paul kujiunga na Ukristo baada ya tukio la safari yake ile, linaegemea kwenye imani kuhusu ukuu wa Mungu, na aliendelea kumtukuza huku akilitangaza neno lake kwa wanadamu.
Wanasayansi wanalinganisha maelezo yaliyomo kwenye Biblia kuhusu tukio hilo la Mtume Paul na lile la kimondo cha nchini Urusi la mwaka 2013, hivyo kuhitimisha kuwa kilichomtokea ni kuanguka kwa kimondo pia. Pamoja na ulinganisho wa matukio hayo mawili, wanasayansi wanatumia maelezo kuhusu mwanga kutoka mbinguni, kama inavyoelezewa kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume, mlango wa tisa,http://onlinelibrary.wiley.com/doi/10.1111/maps.12428/abstract(link is external), na kutoa maelezo yao ya kisayansi katika tukio hilo la Mtume Paul.
Wanasayansi kwa upande wao wanaliangalia tukio lile kisayansi zaidi. William Hartmann, mmoja wa waanzilishi wa taasisi ya “Planetary Science Institute in Tucson, Arizona,” anatoa maelezo tofauti kuhusu kilichomtokea Mtume Paul katika safari yake hiyo ya Damascus, kwamba hakikuwa kitu kingine zaidi ya kishindo cha kimondo kilichokuwa kikianguka, kikiambatana na mwanga mkali.
Wataalamu hao wa masuala ya unajimu, wanabainisha mwanga aliouona ndio uliomsababishia upofu, wa muda, kwani baadaye alirudiwa na nguvu zake za kuona.
Kimondo cha Mbozi
Taarifa kwenye mtandao wa Wikipedia, https://en.wikipedia.org/wiki/Mbozi_meteorit(link is external), zinabainisha kuwa kimondo cha Mbozi ni miongoni mwa vimondo nane vikubwa duniani na katika kundi hilo kinashika nafasi ya nne.
Kuna taarifa zinazopishana kuhusu vipimo vya Kimondo cha Mbozi, hata hivyo katika mtandao huo wa Wikipedia inaonyeshwa kuwa kimondo hicho kina urefu wa mita tatu na kimo cha mita moja, huku uzito wake ukikadiriwa kuwa tani 16.
Taarifa ya Mkuu wa Kituo, Mhifadhi Filmerick Basange inaoana na ile iliyopo kwenye mtandao huo kuhusu urefu na kimo, lakini zinatofautiana kwenye uzito ambapo Mhifadhi huyo anasema kimondo hicho kina uzito wa tani 12, ikiwa ni pungufu na zile za kwenye mtandao huo kwa tani nne.
Maelezo ya wenyeji, yaliyopo kwenye kituo hicho, yanamtaja mhunzi hariri kuwa mtu wa kwanza kutoa taarifa za uwepo wa kimondo hicho kwa Mtawala wa eneo hilo, wakati huo, Chief Mwamengo. Hata hivyo, hakuna aliye na uhakika wa mwaka kilipoanguka pamoja na na ule wa kutolewa kwa taarifa hiyo ya kwanza kuhusu uwepo wa chuma hicho kama ilivyotolewa na mhunzi huyo.
Mpima ardhi (land surveyor), W.H. Nolt kutoka Johannesburg nchini Afrka Kusini alifika hapo kwenye kimondo Oktoba, mwaka 1930 na kuwa mtu wa kwanza kuutangazia ulimwengu kuhusu uwepo wa kimondo hicho, hapo kwenye mteremko wa Mlima Marengi uliopo katika Kijiji cha Ndolezi, Kata ya Mlangali, Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya.
Kimondo cha Mbozi kinawekwa katika kundi la vimondo vya chuma kikiwa na asilimia 90 ya madini hayo. Hata hivyo kinachoshangaza wenyeji na hata wataalamu ni hali ya eneo kilipo kutokuwepo kwa shimo kubwa au kwa lugha nyingine kasoko au crater kwa Kiingereza.
Maelezo ya kisayansi kuhusu utata, meteoritecrater.com, huo yanabainisha kuwepo kwa sababu za kisayansi zaidi katika umbaji wake.
Hupati tabu sana kukifikia kimondo cha Mbozi. Kinafikika kirahisi kwa kutumia usafiri wa gari, pikipiki, bajaji na hata baiskeli.
Kimondo hicho kinafikika kwa urahisi utokapo jijini Mbeya au Mji wa Tunduma, mpakani mwa Tanzania na Zambia. Kwa kutokea jijini Mbeya, ni kilometa 40 kwa njia ya Barabara Kuu iendayo nchini Zambia, hadi kufika njia panda, kisha unafuata barabara ya vumbi upande wa Kusini ambapo ni mwendo wa kilometa tisa hadi kukifikia.
Jambo la msigi na haraka katika kukiedeleza kimondo cha Mbozi, ni kuanzishwa kwa Makumbusho na Kituo cha Utafiti wa Masuala ya Unajimu (astronomy) ili eneo hilo liwe kitivo cha elimu ya vimondo na unajimu barani Afrika na kuitangaza imani hiyo ya wenyeji ya kuosha nyota.
Muonekano mungine wa kimondo hichi cha mbozi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni