GETRUDE Clement (16) ni mtoto wa
Kitanzania kutoka Mtandao wa
Wanahabari Watoto mkoani Mwanza,
ambaye anakuwa mmoja wa watoto
wachache kuhutubia kwa kujiamini kwa
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
lililokutana jijini New York nchini
Marekani hivi karibuni.
Mtoto huyo anayesoma kidato cha tatu
katika shule ya sekondari ya Mnarani
amekuwa gumzo katika sehemu
mbalimbali duniani, kutokana na hotuba
yake aliyotoa kwa kujiamini mbele ya
marais na viongozi wanaoongoza nchi
wanachama wa baraza hilo. Ni katika
mkutano huo uliohudhuriwa na marais
60 na viongozi wengine wa mataifa
zaidi ya 150 uliohusu masuala ya
Mabadiliko ya Tabianchi, ambapo
mataifa zaidi ya 150 yalitia saini
makubaliano ya kukabiliana na
mabadiliko hayo ikiwemo Taifa la
Marekani.
Awali kabla ya kusoma hotuba yake,
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban
Ki moon alimkaribisha Getrude kwa
kusema; “ni furaha yangu kumualika
Getrude Clement ambaye pia ni
mwakilishi wa vijana anayeishi
Tanzania ambaye anawakilisha sauti za
vijana.” Baada ya kufika mbele ya
viongozi hao, aliwasalimia na
kuwaeleza kuwa yeye ni mwakilishi wa
vijana na watoto duniani katika
kuzungumzia mabadiliko ya tabia nchi,
ambapo alielezea hatari yake na
kwamba amekuwa akifanya kazi ya
kufikisha ujumbe huo kwa wananchi juu
ya mabadiliko hayo.
Mchango wa wazazi Akizungumza na
Blogu hii baada ya kurejea nchini wiki
hii, Getrude ambaye ni mtoto wa pili
kuzaliwa katika familia ya Clement
Leon na mke wake Riziki Athumani
wakazi wa Pasiansi mkoani Mwanza
yenye watoto watano, anasema
kujiamini kwake kumetokana na wazazi
wake na ndugu zake kuwa karibu naye.
Wazazi na ndugu hao kwa mujibu wa
Getrude, wamekuwa wakimuunga
mkono kwa yale anayofanya bila
kumkatisha tamaa jambo ambalo
limekuwa likitia chachu katika jitihada
zake binafsi kila wakati.
Anasema alipata fursa ya
kuwawakilisha vijana na watoto
kutokana na kuwa mwanahabari mtoto
wa mkoani humo, ambaye amekuwa
akifanya vipindi vya watoto katika
runinga na redio. Getrude anasema
yeye pia ni mwanachama wa Mtandao
wenye programu zinazozungumzia
mabadiliko ya tabia nchi kwa
kutembelea sehemu zilizoathirika na
kuzungumza na viongozi wa maeneo
hayo.
Anasema ili kupata njia nzuri ya
kukabiliana na mabadiliko hayo,
wanachama wa kikundi hicho pamoja
na viongozi wa maeneo husika kwa
pamoja, hufanya vipindi katika redio au
runinga na kupata maoni ya watu. Binti
huyo anasema pia kikundi hicho kwa
kushirikisha maoni yao, wamekuwa
wakiwaeleza namna bora ya
kukabiliana na mabadiliko ya tabia
nchi.
Anasema hotuba hiyo aliyoitoa UN,
aliiandaa mwenyewe katika Baraza la
Watoto mkoani Mwanza, baadaye
ikafanyiwa marekebisho na watu
mbalimbali wakiwemo viongozi wake
wa baraza hilo. Mwanafunzi huyo
anayetoka shule ya Serikali, ambazo
zimekuwa zikituhumiwa kushindwa
kutoa elimu bora, anasema mwalimu
mzuri wa somo la Kiingereza na
ufuatiliaji wake wa masomo hayo,
vimemwezesha kusoma kwa umakini
hotuba ile ingawa si kwamba anajua
sana lugha hiyo bali alikuwa akiisoma
mara kwa mara.
Hotuba hiyo kwa mujibu wa binti huyo,
haikuandaliwa muda mrefu kwani
aliandika mwanzoni mwa Machi mwaka
huu kisha kufanyia mazoezi ya mara
kwa mara wakati alipokuwa na uhakika
wa kwenda kuisoma mbele ya viongozi
hao wakuu.
“Kwa kweli niliambiwa kuwa nitasoma
kwa viongozi wakuu lakini sikujua kama
watu watakuwa wengi kiasi kile kiasi
ambapo mara baada ya kutangazwa
kusoma hotuba nilipata hofu lakini kadri
nilivyokuwa nikiendelea kuisoma, niliona
nawasomea watu wa kawaida,”
anasema kwa kujiamini. Anasema tabia
yake ya kutokuwa na hofu, imetokana
na kujiamini kwani amekuwa akifanya
vipindi mbalimbali vya watoto na
amekuwa na jitihada za kuhakikisha
anafanikiwa kwa kila kilicho mbele
yake.
Akizungumzia mipango yake ya
baadaye, Getrude anayesema anapenda
masomo ya sayansi, anasema
anapenda kuwa Mtangazaji wa
kimataifa kwa kuwa anapenda kazi hiyo
anayofanya kila wakati na tayari
ameshaanza kukabiliana na
changamoto zake akiwa mtoto.
Anamtaja mtangazaji anayemvutia
kuwa ni Salim Kikeke wa Shirika la
Utangazaji la Uingereza (BBC) na
wengine wengi wa nchini huku
akisisitiza kuwa kazi hiyo imemfanya
afanikiwe kushiriki masuala mbalimbali
katika jamii.
Ushauri kwa watoto, wazazi Anawataka
watoto nchini kufuata kila
wanachoelekezwa na walimu au wazazi
wao kwa kuwa na nidhamu huku
wakishiriki katika makundi mbalimbali
ya watoto na vijana. “Makundi haya
licha ya kukuongezea ufahamu, pia
yatakupa fursa mbalimbali za kukutana
na watu mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kupata fursa za kukuwezesha kujiamini
zaidi,” anasisitiza.
Anasema pia wazazi wanapaswa kuwa
karibu na watoto na kuwaruhusu
kushiriki katika makundi mbalimbali,
kwani wazazi wana nafasi kubwa ya
kuwafanya watoto wawe wa aina fulani
ikiwa ni pamoja na kuwaepusha
kushiriki katika makundi mabaya.
Ushauri kwa Serikali Getrude anaishauri
Serikali ya Tanzania kuanza kuchukua
hatua kwa kushirikiana na wananchi
wake kuwapa elimu ya kutosha kuhusu
mabadiliko ya tabia nchi na hiyo ndiyo
itakuwa zawadi kubwa kwake kama
mwakilishi wa nchi.
“Hii itanifanya nijione yale niliyowataka
viongozi wayafanye, yamefanyiwa kazi
kwa uhakika lakini nahisi haya
yatafanyiwa kazi na nchi zote kutokana
na mwitikio wa viongozi hao niliopata
mara baada ya kusoma,” anasisitiza.
Mtoto huyo aliyerejea wiki hii kwa
wazazi wake mkoani Mwanza alipata
mapokezi makubwa huku akieleza kwa
jinsi vyombo mbalimbali vya habari vya
kitaifa na kimataifa walivyomtafuta na
kumhoji.
Watanzania wametoa pongezi nyingi
kwa Getrude na kusema ni hazina ya
nchi, hadi sasa kwani amesaidia
kuitangaza nchi duniani kutokana na
hotuba hiyo aliyotoa mbele ya Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ki-moon.
Akizungumzia safari yao, Katibu Mkuu
wa Shirika la Mtandao wa Watoto na
Vijana Mwanza, Brightius Titus
anasema walimuandaa vizuri mtoto
huyo kwa kufanya mazoezi katika
ukumbi huo siku moja kabla ya
mkutano.
Anasema mara baada ya kutoa hotuba
hiyo watu kadhaa walimfuata
kumpongeza akiwa njiani kuelekea
hotelini na hata alipofika. Titus
anasema nia ya shirika hilo ni
kuendeleza jitihada za mtoto huyo kwa
kumpa nafasi ya kwenda mbele zaidi
na kuwa mfano kwa watoto na vijana
wa Kitanzania. Anamshukuru Balozi wa
Tanzania nchini Marekani kwa kumuita
nyumbani kwake na kumpongeza
pamoja na ofisi ya Makamu wa Rais
iliyomuita katika ofisi hizo mara tu
baada ya kuwasili nchini.